Mwongozo wa gharama za matibabu kuanza kutumika mwaka 2023

0
22

Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuja na mwongozo wa gharama za matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma nchini ambao unatarajiwa kuanza kutumika kuanzia mwezi Februari 2023.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipofanya ziara ya kushitukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke kuona hali ya utoaji huduma za afya pamoja na kusikiliza kero, ushauri na maoni ya wananchi juu ya upatikanaji wa huduma za afya nchini.

“Kero ya watu wengi hapa ni gharama za matibabu, tumepokea maoni ya wananchi, hospitali zetu wamejiwekea gharama bila hata kupewa mwongozo, sasa hivi wizara inakamilisha mwongozo wa uchangiaji gharama za matibabu na utaanza kutumika mwezi Februari 2023,” ameeleza.

Ameongeza kuwa sera ya afya ya mwaka 2007 inaelekeza wananchi kuchangia gharama za matibabu, hivyo kupitia mwongozo huo utatoa mchanganuo wa gharama za kumuona daktari kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali ya Rufaa, Wilaya, Mkoa, Kanda, Maalum na Taifa.

Waziri Ummy amesema hapo awali hakukuwa na mwongozo unaoainisha gharama husika za kumuona daktari hivyo kupelea vituo vingi vya kutoa huduma za afya kuwa na gharama tofauti tofauti zisizoendana hivyo kuleta kero zaidi kwa wananchi.