Mtanzania Elizabeth Mrema ateuliwa kuongoza shirika la Umoja wa Mataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amemteua Elizabeth Maruma Mrema kutoka Tanzania kuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP).
Bi. Mrema atamrithi Joyce Msuya kutoka Tanzania aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Masuala ya Kibinadamu na Naibu Mratibu wa Misaada ya Dharura katika ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA).
Elizabeth amehudumu katika nafasi mbalimbali ambapo tangu mwaka 2020 amehudumu kama Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Bayoanuai (CBD), yenye makao yake mjini Montreal, Canada.
Hapo awali aliwahi kuwaKaimu Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya CBD na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika shirika la UNEP huko Nairobi, Kenya, pamoja na kuwa Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Mkataba wa Sekretarieti ya Wanyama Wanaohama yenye makao yake makuu mjini Bonn, Ujerumani.
Guterres amesema akiwa anahudumu zaidi ya miongo miwili katika Umoja wa Mataifa, Bi. Mrema ameleta uzoefu mkubwa katika sheria ya kimataifa ya mazingira na utungaji sera, utekelezaji wa programu za mazingira na maendeleo endelevu na ujuzi wa kina katika usimamizi na uongozi wa michakato ya kimataifa ya mazingira.
Kabla ya kujiunga na UNEP mwaka 1994, Bi. Mrema alifanya kazi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania kama Mshauri na Wakili Mwandamizi wa Kisheria.
Akiwa wizarani, aliwahi pia kuwa Mhadhiri wa masuala ya sheria ya kimataifa ya umma na diplomasia ya mikutano katika kituo cha ushirikiano wa masuala ya nje na diplomasia cha Tanzania.
Mrema ana shahada ya uzamili ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dalhousie, Halifax, Canada, stashahada ya uzamili ya uhusiano wa kimataifa na diplomasia kutoka kituo cha uhusiano wa nje na diplomasia cha Dar es Salaam Tanzania na shahada ya kwanza ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.