TAMISEMI: Hakutakuwa na uhamisho wa wanafunzi kwenda shule za bweni 

0
38

Serikali imesema hakutakuwa na uhamisho wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule za kutwa kuhamia bweni.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Prof. Riziki Shemdoe jijini Dodoma katika kikao cha kufanya tathimini ya usimamizi na uendeshaji wa elimu nchini kwa mwaka 2022 kwa Maafisa Elimu wa Mikoa.

Amesema tangu Waziri wa TAMISEMI, Angellah Kairuki atoe taarifa ya kuwapangia shule wanafunzi wa kidato cha kwanza 2023, TAMISEMI  imepokea maombi mengi kutoka kwa wazazi kuomba watoto wao kuhamia shule za bweni kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za ugonjwa au matamanio ya wazazi.

Kutokana na hali hiyo, Prof. Shemdoe amesema hakuna uhamisho wa wanafunzi waliochaguliwa kutwa Kwenda bweni kwani upangaji umefuata vigezo na utaratibu.

“Na kwa wanafunzi wenye changamoto za kimazingira, mfano amehama makazi ya awali wawasilishe changamoto hizo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ili zitatuliwe maana upangaji wa wanafunzi kwenye shule umezingatia ukaribu wa shule na makazi ya wanafunzi hivyo endapo wamehama makazi ya awali kunaweza kutokea changamoto ya umbali,” amesema.

Ameongeza kuwa idadi ya wanafunzi waliopangiwa kwenye shule za bweni imezingatia viwango vya juu vya ufaulu na nafasi zilizokuwepo katika shule hizo ili kuepusha msongamano kwa wanafunzi darasani na mahali pa kulala.

Send this to a friend