Rais Samia Suluhu Hassan ameondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa nchini akieleza kuwa ni haki kwa vyama hivyo kufanya mikutano hiyo, huku akivitaka kufanya siasa za kistaarabu.
Ameyasema hayo leo Januari 03, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na kuzungumza na viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa nchini ambapo amesema wajibu wa vyama vya siasa ni kufuata sheria na kanuni zinavyosema pamoja na kufanya siasa za kujenga na si kubomoa.
“Nimekaa na vyombo vyangu vya ulinzi na usalama na nitakaa nao tena, kazi yetu ni kuwalinda, [..] lengo letu, kazi yetu ni kuja kuwalinda kwenye mikutano yenu,” ameeleza.
Aidha, amesema Serikali inadhamiria kukwamua mchakato wa marekebisho ya katiba ambapo hivi karibuni itaunda kamati ya ushauri ambayo itahusisha Watanzania wa sekta na nyanja zote.
Ameongeza kuwa katiba zinazopendekezwa ni za muda mrefu ambapo baadhi ya mambo yamebadilika, hivyo kuna haja ya kuangalia hali halisi ya sasa ikoje na hata kuanza na katiba iliyopo ili kuichambua yapi yanayofaa na yapi yarekebishwe, pamoja na kuchukua baadhi mazuri kutoka kwenye katiba zinazopendekezwa.