Taarifa ya TCRA kuhusu vocha za simu ‘kupandishwa’ bei

0
24

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabir Bakari amesema hakuna vocha zilizopanda bei, na kama zipo ni utapeli ambao unapaswa kuchukuliwa hatua.

Amebainisha hayo wakati wa mahojiano na gazeti la Mwananchi juu ya vocha za kukwangua za mitandao mbalimbali ambazo zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya juu pasipo mamlaka husika kupandisha bei hizo.

“Hakuna bei iliyopanda, kama umepandishiwa nenda katika ofisi maalum [ya mtandao husika] ukaripoti au ukanunue kwenye maduka yao ya mawakala, kama vishoka wamekupiga nenda polisi,” amesema Dkt. Bakari.

Aidha, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando amesema hakuna sehemu yoyote waliyoongeza bei za vocha tofauti na zilizotangazwa na kuahidi kuwa wanafuatilia suala hilo.

Vurugu zaibuka kanisani, waumini wamkataa mchungaji mpya

Naye Mkurugenzi wa Biashara wa Vodacom Tanzania PLC, Linda Riwa amesema mtandao huo haujapandisha bei ya vocha na kwamba bei zinazotumika ni zile zile za awali.

Kwa zaidi ya wiki moja, vocha ya TZS 500 inauzwa TZS 550 au 600 na ile ya TZS 1,000 inauzwa kati ya TZS 1,100 hadi TZS 1,200 katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Kilimanjaro.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend