Katambi: Vijana jitoleeni, msisubiri kuajiriwa
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema kilio cha ukosefu wa ajira kwa vijana kitaondoka endapo kundi hilo litabadilisha mtazamo na kuanza kujitambua kwa kufanya shughuli mbalimbali zilizopo katika mazingira yao kabla ya kufikiria kuajiriwa.
Ameyasema hayo Januari 10 wakati wa kongamano la vijana lililofanyika katika Chuo cha Ualimu Kigurunyembe mkoani Morogoro chini ya uratibu wa tawi la Msalaba Mwekundu mkoani humo ambapo amewataka vijana kujenga tabia ya kujitolea katika masuala ya kijamii kwa lengo la kusaidia wengine badala ya kusubiri kuajiriwa.
Mwanafunzi ajiua baada ya kukataliwa na mpenzi wake aliyempa iPhone 14
Katambi amewaeleza vijana kuwa Serikali inaendelea kutengeneza fursa mbalimbali za vijana ili kujikwamua kupitia mafunzo yanayotolewa na taasisi mbalimbali ikiwemo Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania.
Amesema vijana wanapokuwa tayari kujitolea inawasaidia kupata uzoefu katika huduma au msaada wanaotoa na wanasaidia kulijenga taifa badala ya kusubiri kuajiriwa.
“Vijana mlio kwenye chama hiki mnafanya kazi kubwa ni wazi mna moyo wa kujitolea naomba mwendelee kufanya hivyo ili kuweza kusaidia nchi katika maeneo mbalimbali na nawahikikishia kuwa Serikali inaendelea kupambana kwa ajili yenu na Watanzania wote kwa ujumla,” amesema.