Mchengerwa aiagiza kamati kukamilisha Mdundo wa Taifa

0
29

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa ameipongeza Kamati ya Kutafuta Mdundo wa Taifa kwa hatua iliyofikia na kuitaka kukamilisha kazi hiyo mara moja ili uanze kutumika katika soko la Afrika na dunia.

Mchengerwa ameiagiza Kamati hiyo inayosimamiwa na Mtendaji Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dkt. Kedmon Mapana kuainisha wasanii 10 watakaosaidiwa na Serikali ambao wanatumia midundo hiyo kuandaa miziki itakayotambulisha mdundo huo.

Amesema dhamira ya Serikali ni kufanya uwekezaji mkubwa kwa wasanii wengi wa Tanzania ili wafike kwenye ngazi ya kimataifa kama mataifa mengine yanayofanya vizuri duniani.

Aidha, ameitaka Kamati kuandaa mkakati wa kuutangaza mdundo huo wa taifa ili ukubalike na ujulikane ulimwenguni pamoja na kuelekeza kuwa siku ya uzinduzi rasmi wa mdundo wa taifa nyimbo hizo ziwe zimerekodiwa na kutumbuizwa mubashara katika mitandao mbalimbali duniani.

Kwa upande wake mjumbe wa Kamati hiyo, Zahir Ally Zolo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta za Sanaa pamoja na kufanya mapinduzi makubwa katika kipindi kifupi cha utawala wake.

Send this to a friend