Afisa Uhifadhi wa Wanyamapori Daraja la Kwanza wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Deus Mwakajegele ameuawa kwa kuchomwa mshale na watu wasiojulika alipokuwa akitekeleza majukumu yake.
Akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee katika ufunguzi wa wiki ya sheria mjini Musoma amesema tukio hilo limetokea Januari 21, 2023 katika eneo la Nyanungu wilayani Tarime mkoani Mara ambapo afisa huyo alichomwa mshale wenye sumu kichwani na kufariki katika Hospitali ya Selian Arusha alipopelekwa kwa matibabu.
“Nimesikitika sana yani wananchi wamefikia hatua ya kumchoma askari mshale wenye sumu akiwa anatekeleza majukumu yake, hii ni mbaya sana,” ameeleza.
Aidha, Jenerali Mzee amesema tukio hilo limetokea katika eneo ambalo lilikuwa na migogoro na tayari lilikuwa limetolewa maamuzi na vyombo vya dola.