Waziri Nape: Laini ambazo hazijahakikiwa kufungwa Februari 13
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametangaza kuwa laini zote zilizosajiliwa kupitia vitambullisho vya watu wengine zitafungiwa Februari 13, 2023 saa 10 jioni.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Waziri Nape amesema Serikali ina lengo la kuwaondoa matapeli kwenye mfumo hivyo laini zote ambazo hazijahakikiwa, ambayo haitahakikiwa itafungwa.
“Wale wenye laini kahakikini laini kama unazo nne tano kahakiki zote vinginevyo usipohakiki ambayo haitoahakikiwa itafungwa na hatutokuwa na nyongeza ya muda tena tunadhani tukomeshe hii hali ya utapeli,” amesema
Aidha, Waziri Nnauye amesema takwimu ya Januari 19, 2023 inaonesha kuwa jumla ya laini za simu zinazotumika nchini Tanzania ni 60,739,790 na laini zilizohakikiwa ni 58,432,669 sawa na asilimia 96 huku laini zisizohakikiwa zikiwa 2,307,121 sawa na asilimia 3.8