Lissu: Lissu: Katiba mpya itaondoa ugumu wa maisha

0
20

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amesema ugumu wa maisha uliopo nchini ni tatizo la kimsingi la kisiasa, hivyo Watanzania wataondokana na ugumu huo endapo wataungana na kudai Katiba mpya.

Lissu ameyasema hayo leo Januari 25, 2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Bulyaga Temeke baada ya kuwasili kutoka Ubelgiji alipokuwa akiishi kwa miaka mitano.

“Kwa wale wenye katiba kuna kamstari mahali kwenye katiba, kanakoelezea kwanini bei ya maharage ni sawa na bei ya nyama, katiba inampa mamlaka makubwa Rais wa kuamua watu watozwe nini na kwa wakati gani,” ameeleza

Amesema “Tatizo la maisha magumu ni tatizo la utawala, tatizo la kisiasa, tatizo la kikatiba. Kama kweli mmechoka dawa nitakayowapa ni tutafute suluhu la kisiasa, tutafute katiba mpya.”

Aidha, kwa upande wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema mageuzi ya siasa za Tanzania yanapaswa kuanzia Dar es Salaam kwa kuwa ndilo jiji lenye idadi kubwa ya watu na lenye makabila ya watu mbalimbali ukilinganisha na maeneo mengine.

“Kutokana na idadi kubwa ya watu waliopo Dar es Salaam kama wakiamua kudai katiba mpya kwa kushirikiana utafika wakati katiba mpya itapatikana. Mwaka huu tumefungua mikutano, tumerejea leo Dar es Salaam kumpokea Makamu, tutapiga jaramba, huku tunazungumza na kuwaamsha wananchi,” amesisitiza Mbowe.

Lissu amerejea nchini leo tangu alipoondoka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambapo alikuwa mgombea Urais kupitia chama hicho, akichuana na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Send this to a friend