Tanzania na Kenya zakanusha taarifa ya shirika la ndege la KLM

0
17

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amekanusha taarifa zinazoenea kuhusiana na uwepo wa matukio ya kihalifu Dar es Salaam ambazo zimeripotiwa na Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM).

Serikali imesema uvumi huo unaenezwa na baadhi ya taasisi za kigeni, na kwamba Tanzania haina machafuko wala matukio ya kigaidi kama inavyoripotiwa, hivyo wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku.

“Tunapenda kuwahakikishia balozi zote, mashirika ya kimataifa, makampuni, taasisi, wageni na wananchi kwa ujumla kwamba eneo la Tanzania liko salama na hakuna machafuko ya wenyewe kwa wenyewe au tishio la mashambulizi ya kigaidi,” amesisitiza Msemaji Mkuu wa Serikali.

Wakati huo huo, Kenya imepanga kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Uholanzi baada ya KLM kutangaza kusitisha safari zake kwa madai ya hofu ya machafuko.

Ingawa taarifa hiyo iliondolewa baadaye kwenye tovuti ya shirika la ndege, Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Uchukuzi nchini Kenya, Kipchumba Murkomen amesema bado nchi hiyo itafanya mjadala kupitia njia za kidiplomasia ili kuhakikisha kuwa hali hiyo haijirudii tena, akidai taarifa hizo ni za uongo na za upotoshaji zinazoipa nchi hiyo picha mbaya.

Siku ya Ijumaa, KLM katika kurasa zake za mitandao ya kijamii na tovuti rasmi iliorodhesha nchi ya Kenya na Tanzania kama nchi zenye tishio la uhalifu na kuwa litasitisha safari zake kupitia kuja Tanzania na kwenda Kenya hadi Jumatatu Januari 30, 2022.

Send this to a friend