Wanachuo wakamatwa kwa tuhuma za unyanyasaji kijinsia mtandaoni
Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashililia Efron Isaya (32) na Cosmas Robert (26) wote wanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo cha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (CDTI) kwa tuhuma za kutishia kusambaza picha za utupu za mwanafunzi mwenzao wa kike.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema Januari 21 muda wa saa 11:00 jioni kuliripotiwa tukio la unyanyasaji wa kijinsia mwanafunzi wa chuo hicho (jina limehifadhiwa) kwa njia ya mtandao na wanafunzi wenzake.
Masejo amesema baada ya kupata taarifa hiyo jeshi hilo lilianza uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata wanafunzi hao wawili, na upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.