Mhagama: Tunasubiri taarifa juu ya wateule ‘waliogomea’ ukuu wa wilaya

0
13

Kufuatia taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kugoma kula kiapo baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema wanasubiri taarifa rasmi kujua hatua zipi za kuchukuliwa.

Viongozi walioshindwa kuapa ni Rais wa CWT, Leah Ulaya ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita na Katibu Mkuu wa chama hicho, Japheth Maganga aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumanne Januari 31, 2023 amebainisha kuwa taarifa amezipata kwenye vyombo vya habari kuwa wateule hao hawako tayari kula viapo kwa nafasi walizoteuliwa.

“Kwa sababu wale ni viongozi wa chama cha wafanyakazi ambao wanasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu lakini wale ni watumishi ambao wanafanya kazi chini ya Ofisiya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa hiyo tutapata hizo taarifa,” amesema.

Aidha, amesema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Rais amepewa madaraka ya kukasimu majukumu yake ya utendaji wa kazi ndani ya Serikali kwa watu mbalimbali kwa kutumia sifa na vigezo walivyonavyo hivyo kuwateua viongozi hao ni heshima kubwa ambayo anakuwa ameitoa inayoendana na madaraka hayo ya kikatiba.

Send this to a friend