Shirika la Ndege la Precision Air, limetoa msaada wa chakula na mahitaji mengine muhimu kwa vituo vitano vilivyomo Bukoba pamoja na mchango kwa vikundi vya wavuvi vilivyopo kando ya Ziwa Victoria.
Akizingumza katika tukio la kukabidhi msaada huo pamoja na mchango, Mkurugenzi Mkuu, Patrick Mwanri amesema wameamua kufanya hivyo ikiwa ni ishara ya kusema asante kwa Mwenyezi Mungu pamoja na wakazi wa Bukoba kwa kuwakimbilia wakati wa ajali ya ndege.
“Hatuna budi kusema asante kwa namna Mwenyezi Mungu ameendelea kutupatia nguvu na ujasiri kwa wakati wote, na kidogo hiki tunachotoa kinabeba shukrani zetu za dhati.
Ameongeza kuwa pia ushujaa uliooneshwa na wavuvi waliokuwa karibu na eneo la tukio hauwezi kulipwa kwa thamani yeyote ila amewaomba wapokee mchango huo kidogo kama ishara ya kitambua juhudi zao.
Shirika hilo limetoa msaada wenye thamani ya TZS milioni 10 na mchango kwa vikundi vya wavuvi wa TZS milioni 10.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mjini, Erasto Sima amewapongeza Precision Air kwa kufanya jambo la kiungwana na kuwataka kuendelea na moyo huo wa kuwakumbuka wenye mahitaji.
Pia amewatoa hofu wananchi na kuwataka kuendelea kusafiri na Precision Air kwa usafiri huo ni salama na kwamba ajali iliyotokea inaweza kutokea kwa shirika lolote duniani.