Wataalamu mbalimbali wa afya nchini Tanzania wamesema unywaji wa maji kupita kiasi unaweza kuleta athari mbalimbali katika mwili wa binadamu.
Daktari kutoka Hospitali ya Megacare Specialized Polyclinic ya mkoani Arusha, Ahobokile Mwaiswelo amesema kitaalamu maji ni muhimu katika mwili wa binadamu lakini endapo yatatumika kupita kiasi yanaweza kusababisha figo kutofanya kazi vizuri.
“Ukinywa maji mengi figo inaweza kushindwa kuyatoa mwilini na ukapata shinikizo la damu. Pia huleta maumivu makali ya kichwa na kupunguza madini ya chumvi mwilini,” amesema.
Dkt. Mwaiswelo amedokeza kuwa unywaji wa maji unategemea mazingira anayoishi mtu, hali ya hewa na uzito, ambavyo kwa ujumla wake vinaweza kutathmini kiwango cha mtu kunywa maji.
Aidha, daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kutoka hospitali ya Benjamini Mkapa mkoani Dodoma, Remigius Rugakingira ameeleza kuwa maji yanapozidi mwilini husababisha kichefuchefu, kutapika, kupata uzito uliopitiliza na mwili kuvimba.
Ameshauri kuwa mtu anatakiwa kunywa maji kwa siku mara tatu, asubuhi mchana na jioni na kiwango kidogo cha maji mwilini kinaweza kusababisha kupata mawe ndani ya figo, presha kushuka, mdomo kukauka na ngozi kutokuwa na afya.