CUF yamtaka Jaji Biswalo ajiuzulu

0
9

Chama cha Wananchi (CUF) kimemtaka aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga ajiuzulu cheo chake kama Jaji wa Mahakama Kuu kufuatia tuhuma za upotevu wa fedha zilizopatikana kupitia mchakato wa plea bargaining.

Akizungumza Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba amedai ili uchunguzi ufanyike kwa haki, Jaji Biswalo na waliokuwa wasaidizi wake wajiuzulu.

“Hata wale watumishi waliokuwa wakimsaidia Mkurugenzi wa Mashitaka kwa kipindi hicho cha plea Bargaining wasimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi huru wa tume hiyo na uchunguzi wake utakuwa wenye tija na kufuata utawala wa sheria pamoja na kurejesha imani ya Watanzania katika ofisi husika,” ameeleza.

ACT Wazalendo wamtaka Jaji Mkuu na Jaji Biswalo wajiuzulu

Aidha, amesema tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu kuchunguza sakata hilo pia ichunguze kama kuna viongozi na taasisi nyingine zilizohusika, fedha zilizopokelewa taslimu na zilizowekwa kwenye akaunti za benki pamoja na mali zisizohamishika zilizowekwa kama dhamana kwa wale walioshindwa kulipa fedha taslimu kama bado ziko mikononi mwa Serikali au zimerejeshwa kinyemela.

“Wale watakaobainika wamehusika katika sakata hili ama la upotevu wa fedha au matumizi mabaya ya ofisi husika basi wachukuliwe hatua za kisheria ili kuzuia matukio kama haya kujirudia tena. Tuna matumaini tume itafanya kazi kwa uadililfu wa hali ya juu bila wala upendeleo,” ameongeza.