Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limesema vurugu zilizojitokeza jijini humo Jumatano Februari 08, 2023 zikiwahusisha wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu ‘Machinga’ zilitokana na operesheni ya askari mgambo ya kuwazuia wafanyabiashara hao kufanya biashara zao katika maeneo ambayo hayaruhusiwi.
Akifafanua kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Willbroad Mutafungwa amedai wakati askari mgambo wakiendelea na kazi hiyo ndipo kundi la watu ambao wanasadikika kuwa ni Machinga lilianza kurusha mawe ili kuwazuia mgambo.
“Katika kundi hilo la machinga pia wameingia watu wengine ambao bado tunafuatilia, ni vijana wadogo wadogo ambao ni wahalifu pia. Vijana hao walishirikiana na Machinga wakaongeza kundi kubwa wakiwa wanarusha mawe ambayo mawe hayo yameweza kuleta uharibifu kwenye magari,” ameeleza Kamanda Mutafungwa.
Gari lilioibiwa kwenye mradi wa SGR lakamatwa likitafutiwa mteja
Aidha, amesema Jeshi la Polisi liliweza kuwakamata vijana wawili ambao walionekana kuwa viongozi wa maandamano hayo, na mpaka sasa vijana hao wanahojiwa kuhusiana na tukio hilo.
Ameongeza kuwa thamani ya uharibifu kutokana na vurugu hizo bado haujafahamika, huku akidai kuwa hakuna madhara yoyote kwa binadamu yaliyojitokeza mpaka sasa.