Takribani watu 21,000 wamefariki dunia na maelfu ya watu kukosa makazi kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea Jumatatu Februari 6, 2023 nchini Uturuki na Syria.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa hali ya baridi kali inayowakumba walionusurika na tetemeko hilo ambao kwa sasa hawana makazi, maji na chakula, linaweza kusababisha janga la pili kiafya.
Ikiwa ni siku ya nne tangu kutokea kwa tetemeko hilo baya kuwahi kutokea, matumani ya waokoaji kuwapata manusura wakiwa hai yanaanza kufifia huku misaada kutoka mataifa mbalimbali ikiendelea kuongezeka.
Wanawake nchini waongoza kuugua saratani kwa asilimia 70
Kundi la uokoaji la White Helmets limesema msaada uliotolewa na Umoja wa Mataifa uliofika eneo hilo haukuwa na vifaa maalum vya kuwaokoa watu waliokwama chini ya vifusi.
“Hii inatufanya tukatishwe tamaa sana wakati ambapo tunatamani sana vifaa kama hivyo vya kutusaidia kuokoa maisha kutoka chini ya vifusi,” kundi hilo lilisema kwenye mtandao wa Twitter.
Siku ya Alhamisi Benki ya Dunia iliahidi msaada wa $1.78 bilioni [TZS trilioni 4.1] kwa Uturuki ikiwa ni pamoja na fedha za haraka kwa ajili ya kujenga upya miundombinu ya msingi na kusaidia wale walioathiriwa na tetemeko la ardhi.