Dkt. Slaa: CHADEMA imekomaa kushika nchi

0
36

Kwa takribani miaka nane baada ya kuondoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA na baadaye Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbroad Slaa amesema anaimani chama hicho sasa kimekomaa kushika dola.

Amesema hayo wakati akiwasalimia wakazi wa Kata ya Rhotia wilayani Karatu mkoa wa Arusha alipohudhuria mkutano wa CHADEMA Februari 27, 2023 uliofanyika katika eneo hilo ambao ulikuwa ukijadili mambo kadhaa ikiwepo mgogoro wa maji katika Mji wa Karatu.

Dkt. Slaa amesema katika kipindi cha awamu ya tatu cha Hayati Rais Banjamin Mkapa wakati akizindua baadhi ya majengo ya Hospitali ya Wilaya Karatu, alimsomea tafsiri ya sera za CHADEMA kisha Rais Mkapa aliomba kitabu cha sera za chama hicho na baadaye kutangaza sera ya afya ya Tanzania nzima kwa kufuata sera ya CHADEMA.

“Kama sera ya CHADEMA inapokelewa inageuka kuwa ndiyo sera ya Taifa, ni kwanini CHADEMA wasifikie hatua ya kuweza kutangazwa kwamba hiki ni chama kikuu na kina uwezo wa kuiongoza Taifa? Matokeo yake tunakuja kuona wananyimwa hata haki ya kufanya mikutano,” ameeleza Dkt. Slaa.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Karatu, Wakili Samweli Welwel amesema bado chama hicho hakijampokea rasmi Dkt. Slaa kurudi CHADEMA na kwamba walimpa fursa kuzungumza na wananchi wa Rhotia ili awasalimie.

Dkt. Slaa aliondoka CHADEMA akiwa Katibu Mkuu wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 baada ya chama hicho kumteua Edward Lowassa kugombea urais, na tangu alipotangaza kujiondoa CHADEMA alikuwa hajapanda kwenye jukwaaa la chama hicho.

Send this to a friend