Kampuni ya  Elon Musk kununua madini kutoka Tanzania

0
40

Kampuni ya Tesla inayomillikiwa na tajiri namba moja duniani, Elon Musk imeingia kwenye ununuzi wa malighafi zinazozalishwa katika migodi ya uchimbaji wa madini ya Graphite (kinywe) yanayopatikana nchini.

Malighafi hiyo inatambuliwa kwa jina la kitaalamu kama Anode Active Material (AAM).

Kampuni hiyo inayotengeza magari, akili bandia  (AI) na uzalishaji wa nishati safi, imesaini mkataba na kampuni zinazochimba madini hayo nchini ili kununua malighafi hizo zinazotokana na madini ya kinywe yanayozalishwa katika mgodi iliyopo mkoani Lindi.

Tesla imesaini mikataba na kampuni ya kimataifa ya uzalishaji wa Betri  ya Magnis Energy Technologies Limited pamoja na kampuni zake tanzu ya Uranex Tanzania Limited (Uranex) na Magnis Technologies Tanzania Limited (MTT) na mkataba huo utadumu kwa miaka mitatu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kampuni ya Uranex imebainisha kuwa chini ya makubaliano hayo yenye thamani isiyojulikana, Tesla imekubali kununua malighafi hizo kutoka Magnis Energy Technologies kati ya tani 17,500 hadi tani 35,000 kwa mwaka kuanzia Februari 2025.

“Mkataba unafika katika wakati muhimu ambapo kwa kampuni zote mbili. Tanzania kama nchi inatazamiwa kufaidika pakubwa katika masuala ya uhamishaji wa teknolojia, ajira, miongoni mwa mambo mengine,” imesema Uranex katika taarifa yake.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend