AJALI: Polisi kukagua shule za udereva na namna madereva walivyopata  leseni

0
30

Katika mkakati wa kupambana na wimbi la ajali nchini, Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limesema limekuja na mkakati wa kuangalia upya shule zote za udereva nchini na kuona namna mafunzo yao yanavyotolewa ili kujiridhisha kama yanakidhi haja pamoja na mazingira mazima ya ufundishaji .

Akizungumza na Swahili Times Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’anzi amesema ametoa maagizo kwa wakuu wa usalama barabarani kufanya operesheni maalum katika mikoa yao ili kubaini shule zote za udereva endapo zina waalimu wanaokidhi pamoja na dhana za ufundishaji, na kwamba shule zote ambazo hazitokuwa na sifa zitafutiwa leseni.

Aidha, amesema kuanzia Machi 08, 2023 kila dereva anapaswa awasilishe leseni yake hasa kwa leseni kubwa za madaraja C na E, kwa wakuu wa usalama barabarani kwa ajili ya ukaguzi, na pia madereva wa magari na malori makubwa wanatakiwa kutembea na vyeti vyao halisi (orijino) kutoka vyuo walivyosomea.

“Dereva atakayebainika leseni yake aliipata kinyume na taratibu atapokonywa, atafutiwa madaraja yake na atatakiwa kwenda kusoma upya na baadaye atatahiniwa,” amesisitiza.

Kamanda Ng’anzi amebainisha kuwa karibia asilimia 80 hadi 90 ya vyanzo vya ajali zinazotokea nchini zinasababishwa na uzembe wa madereva wenyewe na wala si miundombimu iliyopo, hivyo Jeshi la Polisi linafuatilia ni namna gani madereva wamepata leseni zao pamoja na kuangalia uwezo wao wa kiakili, uwezo wa kuona na utimamu wa mwili na saikolojia.

Ameongeza kuwa baadhi ya abiria wanaokemea madereva wanaoendesha kwa mwendo kasi wamekuwa wakikatishwa tamaa na baadhi ya abiria wengine wanaoshabikia vitendo hivyo na kuwachukulia kama adui, hivyo ametoa rai kwa abiria hao kutuma ujumbe mfupi wa maneno na jeshi litachukua hatua mara moja.

Send this to a friend