Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema Afrika Kusini inafikiria kununua umeme kutoka nchini Tanzania ili kusaidia katika kutatua tatizo la nishati nchini humo.
Ameyasema hayo wakati wa mkutano na Rais Samia Suluhu Hassan katika Majengo ya Muungano mjini Pretoria Alhamisi Machi 16, 2022 ikiwa ni sehemu ya ziara ya Kiserikali ya Rais Samia na kikao cha pili cha Tume ya Pamoja ya Afrika Kusini na Tanzania.
“Tulisema tulipotoa mpango wa utekelezaji wa nishati mwaka jana mwezi Julai ni kwamba moja ya mipango tunayoenda kuanza ni kupata nishati ya ziada kutoka kwa majirani zetu. [..] Tulikuwa tumenunua megawati 300 na sasa tulikuwa tunaenda kuongeza kiwango hicho hadi juu kidogo. Nimekuwa nikizungumza na viongozi katika nchi mbalimbali, wanasema tuna ziada kidogo na tunaweza kukuuzia,” amesema Ramaphosa.
Aidha, Rais Ramaphosa ameongeza kuwa ana imani kwamba mzozo wa nishati nchini Afrika Kusini hautazuia uwekezaji nchini humo.
Mkutano huo umeeleza azma ya Tanzania na Afrika Kusini katika kuimarisha uhusiano uliopo wa kisiasa na kiuchumi baina ya nchi hizo mbili pamoja na kuimarisha Tume ya Pamoja (BNC).