Rais Samia amteua Mizengo Pinda kuongoza baraza la kumshauri kuhusu kilimo

0
27

Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kukuza Kilimo na Kuongeza Uzalishaji wa Chakula.

Mbali na Pinda, wajumbe wa baraza hilo ambalo litakuwa na jumuku la kumshauri Rais kuhusu utekelezaji wa masuala ya kilimo na chakula ni Geoffrey Kilenga, Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT na Andrew Masawe, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo.

Aidha, Rais ameteua wajumbe wa sekretarieti ya baraza ambao ni pamoja na Dkt. Florence Turuka, Mhadhiri wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Dkt. Jacqueline Mkindi, Mkurugenzi Mtendaji Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Matunda Tanzania (TAHA) na Dkt. Mwatima Juma, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM).

Rais Samia amesema nia ya Serikali ni kushirikiana na nchi za Afrika kutekeleza azma ya kujitosheleza kwa chakula kwa mujibu wa makubaliano katika mkutano uliofanyika Februari 25 hadi 27, mwaka huu uliokutanisha wakuu wa nchi za Afrika.

“Sasa ni matumaini yangu kwamba kwa kuzingatia uzoefu mlionao nyote wajumbe wa baraza lakini pia sekretarieti mtakwenda kukuza sekta hii na kwamba Rais amepata washauri proper [bora] wa kunishauri kwenye sekta hii,” amesema

Baadhi ya majukumu ya baraza hilo ambayo Rais ameyataja ni kufanya tathmini ya mikakati ya kuinua sekta ya kilimo na kushauri njia bora ya kuitekeleza, kushauri njia na mbinu bora za kuibua na kuendeleza ubunifu wa ndani katika eneo la upatikanaji wa chakula nchini.

Jukumu jingine ni kushauri njia bora ya kuimarisha sekta ya fedha na kuwezesha upatikanaji wa mitaji na fedha kwa wawekezaji na wakulima nchini.

Send this to a friend