Thamani ya uwekezaji nchini yakua kufikia TZS trilioni 19

0
30

Takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zimeonesha thamani ya uwekezaji uliofanyika nchini katika kipindi cha miaka miwili imeongezeka kwa asilimia 173.

Ripoti hiyo inaonesha kiasi kilichowekezwa nchini kilipanda hadi dola bilioni 8.64 (TZS trilioni 20.21) katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kutoka dola bilioni 3.16 (TZS trilioni 7.4) miaka miwili iliyopita kabla ya kuingia madarakani.

Hatua hiyo imetokana na mtazamo wa Rais Samia wa kuunga mkono biashara na uwekezaji ambao umerejesha imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya Machi 2021 na Februari 2023 idadi ya miradi iliyosajiliwa na ambayo fedha hizo ziliingizwa, ilipanda kutoka 455 hadi 575 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 26.

Kamati ya Bunge yashauri barabara ya Kimara-Kibaha iwekewe tozo

TIC imesema kati ya miradi iliyosajiliwa chini ya utawala wa sasa, asilimia 32 inamilikiwa na Watanzania, asilimia 41 ya wageni na asilimia 27 ni ya ubia kati ya wawekezaji wa ndani na nje.

Aidha, kutokana na uwekezaji huo, ajira zilizotolewa zimeongezeka kutoka 61,900 hadi 87,187.

Sekta zilizovutia uwekezaji zaidi katika miaka miwili iliyopita ni uzalishaji wa viwandani kwa asilimia 49.43, ujenzi wa majengo ya biashara kwa asilimia 17.51 pamoja na usafirishaji kwa asilimia 11.07.

“Uboreshaji wa mazingira ya biashara kupitia mpango wa mageuzi ya udhibiti unaendelea, na hii inaweza kuthibitishwa na ongezeko la uwekezaji nchini” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Send this to a friend