Utafiti: Mkoa wa Kilimanjaro unaongoza kwa uzito uliopitiliza na Kiribatumbo 

0
33

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hali ya uzito uliozidi na uzito uliokithiri (kiribatumbo) umeendelea kuongezeka kutoka asilimia 11.3 mwaka 1991 hadi kufikia asilimia 31.7 mwaka 2018 kwa Tanzania Bara huku Zanzibar uzito uliozidi ukifikia asilimia 41.8 katika kipindi hichohicho.

Akizungumza katika uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona, katika Manispaa ya Mtwara amesema tatizo la uzito uliozidi na kiribatumbo ni kubwa katika Mikoa ya Kilimanjaro ambako wana asilimia 49, Dar es Salaam asilimia 48.6, Mjini Magharibi asilimia 47.4 na Kusini Unguja asilimia 39.4.

“Hali hii inaelekea kuwa janga la kitaifa na kisababishi kikubwa cha kuongezeka baadhi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, saratani na magonjwa ya moyo, Wananchi wenzangu, sasa ni wakati mwafaka wa kubadili mitindo ya maisha yetu kwa kufanya mazoezi angalau nusu saa kila siku na kula mlo kamili sambamba na kuepuka vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi, pombe na sigara,” amesema.

Mbali na hayo, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa mikoa 12 wachukue hatua stahiki kutatua tatizo la udumavu uliozidi wastani wa kitaifa kwenye mikoa yao pamoja na kuhimiza lishe bora.

“Mikoa yenye kiwango kikubwa cha udumavu zaidi ya wastani wa kitaifa ni pamoja na Iringa inayoongoza kwa asilimia 56.9, Njombe asilimia 50.4, Rukwa asilimia 49.8, Geita asilimia 38.6 Ruvuma asilimia 35.6, Kagera asilimia 34.3, Simiyu asilimia 33.2, Tabora asilimia 33.1, Katavi asilimia 32.2, Manyara asilimia 32, Songwe asilimia 31.9 na Mbeya asilimia 31.5. Viongozi wa Mikoa hii waitafakari hali hii na kuchukua hatua stahiki,” amefafanua

Send this to a friend