Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa wito kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwajibika kwa hasara iliyojitokeza ya ubadhirifu wa fedha katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya miaka miwili ya mwaka wa fedha 2020/21 na 2021/22.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika katika uchambuzi wa Ripoti ya Mkaguzi na Msimamizi Mkuu wa Serikali (CAG) katika mkutano na waandishi ha habari amesema katika miaka hiyo miwili ya fedha, Waziri Majaliwa alikuwa Mdhibiti Mkuu na Mtekelezaji wa shughuli za Serikali.
“Tungependa kutoa wito kwake kuwajibika kwa udhaifu, ubadhirifu na hasara kwa Serikali iliyofanyika katika miaka hii miwili ya fedha chini ya usimamizi wake wa kila siku kama Mtendaji Mkuu wa shughuli za Serikali,” amesema.
Mapendekezo 10 ya ACT- Wazalendo ripoti ya CAG 2021/22
Aidha, CHADEMA imesema haijaridhishwa na hatua zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuvunja Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kumwondoa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TFGA) kwa kuwa hatua hizo hazijitoshelezi.
“Hatua ya kumwondoa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege [John Nzulule] peke yake ni hatua ambayo ikiachwa ilivyo italenga kufunika kombe bila hatua kamili kuchukuliwa kwenye maeneo makubwa mawili; Ununuzi wa ndege za Serikali, na hasara ya uendeshaji wa shirika la ndege la serikali,” ameeleza
Mbali na hayo amebainisha kuwa mpaka sasa watuhumiwa wa ubadhirifu wa fedha za Serikali katika ripoti iliyopita ya mwaka 2020/21 bado hawajachukuliwa hatua yoyote na kueleza kuwa hawana imani na watuhumiwa waliotajwa katika ripoti ya sasa ikiwa hatua stahiki dhidi yao zitachukuliwa.