Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezielekeza halmashauri zote nchini kusitisha utoaji wa fedha za mikopo kwa makundi maalum ya vijana, wanawake na wenye ulemavu kuanzia Aprili hadi Juni, 2023 wakati Serikali inajipanga kuweka mfumo mpya wa utoaji wa mikopo hiyo.
Ametoa agizo hilo leo akihitimisha hoja zilizotolewa na Wabunge wakati wakijadili Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.
Kumekuwa na changamoto kwenye baadhi ya halmashauri kutoa fedha hizo kwa watumishi wa halmashauri au wakati mwingine vikundi hewa badala ya walengwa na kusababisha fedha za mikopo hiyo kutorejeshwa.
Machi 29, 2023 wakati akipokea taarifa ya ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2021/22 Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kuangaliwa upya kwa utaratibu wa utoaji wa mikopo ikiwemo kuangalia namna ya kutumia mabenki kupitishia mikopo hiyo.