Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Sekiete Yahaya Selemani kuanzia Aprili 16,2023.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu haijaeleza sababu ya utenguzi huo, lakini itakumbukwa kuwa hivi karibuni kulishuhudiwa mvutano kati ya mkurugenzi huyo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima kuhusu uuzaji wa viwanja.
Malima alisema kuwa Sekiete alikuwa amehusika na uuzaji wa viwanja viwili ambavyo vina thamani ya TZS bilioni 1, na kusema kuwa atafikisha suala hilo TAMISEMI ambayo ndio mamlaka yake ya nidhamu.
Serikali yasitisha utoaji mikopo ya 10% katika halmashauri
Katika tuhuma hiyo watumishi wanne akiwemo mhasibu wa Jiji, mwanasheria, ofisa manunuzi na ofisa mipango walifukuzwa kazi baada ya kudaiwa kuuza viwanja vilivyopo mtaa wa kibiashara, katikati ya jiji kwa thamani ndogo kulinganisha na bei ya soko.
Inadaiwa watumishi hao walishirikiana kuuza viwanja hivyo bila kufuata utaratibu kinyume cha taratibu na maadili ya viongozi huku mkurugenzi wa jiji akidaiwa kukiuka maagizo ya kamati ya ulinzi Wilaya ya Nyamagana na ofisi ya mkuu wa mkoa.