Kenya: Mchungaji mshirika wa Mackenzie aachiwa, asema si uchawi ni maombi
Mchungaji Mshirika wa Paul Mackenzie, Ezekiel Odero wa Kanisa la New Life Prayer Center nchini Kenya ameachiliwa kwa dhamana baada ya kushikiliwa kwa wiki moja akihusishwa na mauaji ya zaidi ya watu 100.
Odero ameachiliwa Alhamisi Mei 04, 2023 na mahakama ya Mombasa kwa bondi ya Ksh. milioni 3 (TZS milioni 51) na mdhamini mmoja, au dhamana ya Ksh. milioni 1.5 (TZS milioni 25.9) pesa taslimu.
Mchungaji huyo amepokelewa nje ya ukumbi wa mahakama na umati wa wafuasi wake ambao wamesikika wakiimba “si uchawi, ni maombi” huku wakimwinua hewani.
Mchungaji Odero anatakiwa kuripoti polisi mara moja kila wiki na amezuiwa kutoa maoni yake kuhusu mauaji ya Shakahola.
Masharti ya kuachiliwa kwake yataendelea hadi uchunguzi utakapokamilika na atakaposhitakiwa rasmi mahakamani.
Odero alikamatwa Alhamisi wiki jana akishitumiwa kuwa na uhusiano na mchungaji Mackenzie ambaye anatuhumiwa kwa mauaji makubwa ya wafuasi wake katika kaunti ya Kilifi ambapo zaidi ya watu 100 wamefariki kwa njaa baada ya kudaiwa kutoa maagizo hayo.