Maswali manne ya kuuliza unapotaka kununua gari kwa mtu

0
36

Kumiliki gari ni jambo ambalo vijana wengi wanatamani kutokana na adha ya usafiri hasa kwa jiji la Dar es salam. Kumiliki gari pia kunaweza kukuweka katika changamoto kubwa hasa ikiwa gari ulilonunua limetumika kwa muda mrefu.

Unapofikia uamuzi wa kununua gari hasa lililotumika, unapaswa kuwa makini na kuzingatia kumuuliza maswali ya msingi muuzaji ili usiingie kwenye hasara kubwa baadae.

Baadhi ya maswali unayopaswa kuumuliza muuzaji ni haya;

Kwanini unauza gari?
Ikiwa muuzaji anataka kuuza gari lake, muulize sababu ya yeye kuliuza gari hilo. Namna atakavyojibu swali hili unaweza kupata majibu ikiwa ununue ama la. Kama hawi wazi na majibu yake, basi tambua kuna kitu muhimu anakuficha.

Imetembea kwa kilomita ngapi?
Kama gari hilo limetembea kwa zaidi ya kilomita 32,000/mwaka basi limetumika sana, hivyo linaweza kukuletea matatizo mengi. Vilevile kama halijatembea sana uliza kwanini, labda limepata matatizo mengi likashindwa kutembea kwa muda mrefu.

Ulilinunua likiwa jipya au likiwa limetumika?
Endapo muuzaji alinunua gari likiwa limekwishatumika, ni muhimu kumuuliza mmiliki wa kabla yake aliliuza kwa sababu gani? Kama gari hilo limepita kwa wamiliki wengi kabla yako, inaweza kuwa dalili kwamba linapata matatizo mara kwa mara.

Limewahi kupata ajali?
Ikiwa gari hilo limewahi kupata ajali ndogo basi haina madhara, lakini kama limepata ajali kubwa, ni bora usilinunue.

Majibu ya maswali haya yatakusaidia kuamua kama uko tayari kwa gharama zozote za ziada, ama gari hilo linafaa.
Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend