Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu ‘Musukuma’ ameihoji Serikali juu ya kuendelea kuwepo kwa kampuni inayoendesha mradi wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (SICPA) kwa madai kuwa inaiibia nchi.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma Musukuma amesema kwenye mkataba wa Serikali na kampuni hiyo ulioingia miaka mitatu iliyopita, unasema kila kizibo kimoja cha juice inayotengenezwa Tanzania SICPA inakusanya TZS 8 huku Serikali ikichukua TZS 6.
“Najua wakati mnasaini mkataba mlipunjwa kwasababu labda mlikuwa na viwanda 19, leo tuna mia na kitu. Mfano Azam anachukua karibu milioni 400 kwa siku, makampuni mengine yako Tanzania yanakwambia tuko tayari kuendesha huu mfumo kwa shilingi moja, unang’ang’ania nini kwenye shilingi 8? Amehoji.
Ameongeza, hii kampuni inayochukua kazi hiyo hiyo TZS 8 Tanzania, inafanya kazi Kenya kwa TZS 1 , inafanya kazi Uganda kwa chini ya TZS 1. Sasa mtu huyu bado anaongezwa tena mwaka mmoja, tunaamini kwamba Watanzania hatuna uwezo wa kuendesha huu mfumo.”