Waziri Bashe: Rais Samia ameipaisha Sekta ya Kilimo kimataifa

0
13

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema ni dhahiri kuwa chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kumekuwa na msukumo wa kipekee katika kuendeleza sekta ya kilimo.

Ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati wa hotuba kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2023/2024 ambapo amempongeza Rais Samia kwa kuwa mstari wa mbele katika majadiliano ya masuala ya kilimo kimataifa na kuifanya Tanzania kushinda kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula barani Afrika Septemba mwaka huu.

“Tanzania kuwa mwenyeji wa jukwaa hili, ni fursa kubwa kwa nchi yetu kuvutia uwekezaji katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo na biashara. Nitoe wito kwa wadau wote wa Sekta ya Kilimo hususani sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika jukwaa hilo ambalo litaleta pamoja zaidi ya washiriki 3,000 kutoka nchi mbalimbali duniani,” amesema.

Maelekezo ya Rais Samia kwa Msajili wa Vyama vya Siasa

Aidha, Waziri Bashe amesema Serikali imewawezesha vijana 250 kwenda nchini Israel kwa ajili ya kupata mafunzo ya kilimo kwa vitendo katika mashamba makubwa ili waweze kujiajiri na kutoa huduma na ushauri kwa wakulima watakapohitimu.

Vilevile, amebainisha kuwa Sekta ya Kilimo imechangia asilimia 26.1 katika Pato la Taifa ambapo imetoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda, huku mazao ya kilimo yakichangia takriban Dola za Marekani Bilioni 1.38 ya mauzo nje ya nchi.