Mtoto wa miaka 14 ashtakiwa kwa madai ya kubaka mtoto mwenzake

0
34

Mtoto mwenye umri wa miaka 14 (jina linahifadhiwa) mkazi wa Mji mdogo wa Katoro Wilaya ya Geita mkoani Geita amefikishwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Geita akikabiliwa na mashtaka ya kumbaka mtoto mwenzake mweye umri wa miaka minne.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Nyakato Bigirwa, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Missi Kabula amedai tukio hilo lilitokea Aprili 14, 2023.

Akisoma maelezo ya mashtaka katika shauri hilo namba 87/2023, Wakili Kabula ameiambia mahakama kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa maeneo ya Mchongomani katika Mji Mdogo wa Katoro kinyume cha kifungu namba 130 (1 na 2e) na kifungu namba 131(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Mshatakiwa amekana mashtaka dhidi yake na ameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini hati ya dhamana ya TZS milioni 1.

Serikali yatangaza jina jipya la Hospitali ya Mirembe

Shauri hilo limeahirishwa hadi Mei 24, 2023 itakapotajwa tena huku upande wa mashtaka ukieleza mahakama kuwa upelelezi umekamilika.

Katika shauri nyingine, Abdul Idrisa (46), mkazi wa Msalala Road Wilaya ya Geita amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya jaribio la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 15.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Nyakato Bigirwa, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Missi Kabula amedai kosa hilo lilitendeka Januari 28, 2023 kinyume cha kifungu namba 132(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Shauri hilo namba 89/2023 limeahirishwa hadi Mei 24, 2023 litakapotajwa tena kwa upande wa mashtaka kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali ya kosa.

Mshtakiwa amerejeshwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja anayetakiwa kusaini hati ya TZS milioni 1.

Send this to a friend