Kufuatia taarifa na malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wafanyabiashara wakidai kuwepo kwa urasimu bandarini, hususani katika Bandari ya Dar es Salaam, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekanusha madai hayo.
Katika taarifa yake iliyotolewa Mei 13 mwaka huu imesema kufuatia uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika sekta ya bandari kumekuwa na ongezeko kubwa la kasi ya utoaji huduma hasa upakuaji wa shehena za aina zote hadi kuzikabidhi kwa mawakala wanaokamilisha taratibu za kibandari kwa wakati.
Waziri Ummy asema Serikali inafuatilia tetesi za UVIKO-19
“Katika kuwathamini wateja, TPA inafanya kazi saa 24 kuhudumia shehena aina zote, huku Kitengo cha Huduma kwa Wateja na Kituo cha Mawasiliano ya Simu (Call Centre) vikiwa wazi muda wote wa saa 24 ili kuhakikisha kuwa changamoto zote zinaporipotiwa na wateja na wadau zinapatiwa ufumbuzi wa haraka,” imesema TPA.
Aidha, TPA imesema inawakaribisha wateja na wadau wenye changamoto zozote kuwasiliana na Kurugenzi ya Masoko na Uhusiano ya TPA, au kutumia njia rasmi za mawasiliano za TPA ambazo ni bure pamoja na kutumia kurasa zake za mitatandao ya kijamii katika kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe mara moja.