Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwa mara ya kwanza katika historia, Tanzania imefanikiwa kujenga Ikulu yake kwa kutumia rasilimali zake pamoja na watalaamu kutoka ndani ya nchi tofauti na ikulu ya hapo awali.
Akizungumza katika ufunguzi wa Ikulu mpya ya Chamwino, Dodoma uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali leo, amesema shughuli zote za Serikali sasa zitafanyika mkoani humo ikiwa ni moja wapo ya matamanio ya viongozi wakuu wastaafu akiwemo mhasisi wa taifa, Hayati Julius Nyerere.
“Kazi haikuwa ndogo na ilikuwa ni kazi ya kila awamu iliyoingia kwenye madaraka kuwezesha au kuanza ujenzi wa vitu mbalimbali ili Dodoma ichukue sura ya kuwa makao makuu ya Serikali,” amesema.
Katika kufanikisha mchakato wa kumalizika kwa ikulu hiyo, Rais Samia amempongeza Hayati Dkt. John Magufuli kwa mchango wake mkubwa ambapo utekelezaji wa uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ulipewa msukumo zaidi.
Rais Samia apandisha dau hadi milioni 20 kwa kila goli kwa Yanga
Aidha, Rais Samia ameahidi kuendelea kutekeleza yale yote yaliyoahidiwa pamoja na kuendeleza mazuri yote ili Tanzania iendelee kusonga mbele zaidi kimaendeleo.
“Kama nilivyoahidi nilipokabidhiwa hatamu za uongozi wa nchi yetu kuwa nitaendeleza mema yaliyopo, nitaboresha inapobidi na nitaleta mema mapya kwa misingi ya kaulimbiu ya Kazi iendelee, ameongeza.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete amesema katika kipindi chake cha uongozi walifanya uamuzi wa msingi na wenye tija kwa nchi kukubaliana kwamba Ikulu hiyo ijengwe eneo la Chamwino.
“Katika kipindi changu, uamuzi wa msingi tulioufanya ni kuamua kwamba ofisi ya Rais na makazi ya Rais yatakuwa hapa Chamwino, maana wazo lililokuwepo mwanzoni kwamba pale Chimwaga ndipo patakapokuwa makao makuu ya Chama cha TANU na makao makuu ya Serikali. Mimi nilipokuja nikaamua pale pajengwe Chuo Kikuu,” ameeleza.