Waziri Mbarawa: Miaka miwili ya Rais Samia ni neema sekta ya Ujenzi

0
11

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeweza kupiga hatua kubwa ya mafanikio ikiwemo ujenzi wa barabara na madaraja makubwa ambapo barabara zenye jumla ya kilometa 15,563 ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Waziri wa Ujenzi, Makame Mbarawa akiwasilisha bajetiya mwaka 2023/24, amesema kati ya hizo, barabara zenye kilomita 1,152 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami, barabara zenye jumla ya urefu wa kilometa 1,484 zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 4,141 zimefanyiwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.

“Katika kipindi hicho, wizara imeendelea kutekeleza shughuli na miradi ya reli, barabara, viwanja vya ndege, vivuko, usimamizi wa utengenezaji wa ndege, ujenzi na uboreshaji wa bandari, ujenzi na ukarabati wa meli katika maziwa, na uboreshaji wa vyuo. Hatua hizo zimechochea sekta nyingine za kiuchumi na kijamii katika kuwaletea wananchi maendeleo,” ameeleza.

Rais Samia afanya uteuzi wa balozi

Mbarawa amesema Serikali pia imeanza ujenzi wa awamu ya pili ya reli ya kisasa ya SGR ambapo mkataba wa kipande cha Tabora – Kigoma (km 506) ulisainiwa Desemba 20, 2022 na mkandarasi anaendelea na maandalizi ya vifaa, makambi ya wafanyakazi na kuajiri wafanyakazi.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho ya bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ambapo yamewezesha ongezeko la mizigo inayohudumiwa kutoka tani milioni 1.5  kwa mwezi mwaka 2022 hadi tani milioni 1.93 kwa mwezi mwaka 2023.

“Huduma za bandari zimeweza kuchangia asilimia 43 ya mapato ya kodi ya forodha yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwaka 2021/22 ikilinganishwa na asilimia 37 katika mwaka 2020/21,” ameongeza.

Send this to a friend