Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya utafiti na kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa maandalizi ya kuwa mwenyeji wa Michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Ameyasema hayo Ikulu jijini Dodoma wakati akipokea andiko la ombi la Tanzania, Kenya na Uganda kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON kutoka kwa Rais wa TFF, Wallace Karia pamoja na uongozi wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo.
Katika hatua hiyo, Rais Samia amesema nchi hizo zinawania nafasi hiyo kwa kutambua mafanikio makubwa ambayo sekta ya michezo imepata, hivyo kuwa wenyeji wa AFCON 2027 kutaongeza hamasa zaidi kwa ukuaji wa michezo hususan upande wa soka.
Aidha, amesema michuano hiyo itachangia katika ukuaji wa utalii, kwa kuwa ni mashindano ambayo hutazamwa na zaidi ya watu bilioni moja barani Afrika na maeneno mengi duniani, hivyo yanatarajiwa kunufaisha sekta ya uchumi kwa kupokea wageni mbalimbali na wenye ushawishi duniani.
Mashindano ya AFCON yataweka rekodi kwa mara ya kwanza kufanyika katika Ukanda wa Afrika Mashariki tangu yalipoanzishwa rasmi mwaka 1957.