Wanne washikiliwa kwa mauaji na kukutwa na nyeti za mwanamke
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu wanne akiwemo mganga wa kienyeji kwa tuhuma za ubakaji, mauaji na kukutwa na nyeti za mwanamke katika kijiji cha Bugumangala Wilaya ya Magu mkoani humo.
Akizungumza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Willbroad Mutafungwa amesema jeshi la Polisi lilipokea taarifa za mauaji ya Ester Lukoni (51) mkazi wa kijiji cha Bugumangala Mei 10, mwaka huu ambaye aliuawa kwa kukabwa kisha kukatwa sehemu zake za siri na mwili wake kutelekezwa katika shamba la mihogo.
Mwanafunzi ajiua baada ya kuliwa ada ya chuo kwenye kamari
“Katika tukio hilo ilionekana kuwa marehemu aliingiliwa kimwili kabla ya mauaji hayo ya kikatili, kwani katika eneo la tukio ulipatikana mpira wa kiume (kondomu) ambao ulikuwa umetumika. Tukio hilo lilifanywa na watu ambao hawakuwa wamefahamika kwa wakati ule,” amesema Kamanda Mutafungwa.
Ameongeza kuwa, mmoja wa watuhumiwa hao ambaye ni mganga wa kienyeji alipokea sehemu za siri za marehemu na kuikausha kwa moto kisha akaisaga kwa ajili ya matumizi ya uganga ambayo yalihusisha imani za kishirikina.
Kamanda Mutafungwa amesema watuhumiwa wote waliohusika katika tukio hilo wamekamatwa, na baada ya mahojiano wamekiri kuhusika na ukatili huo.