Gharama ya samaki nchini Kenya kupanda kwa asilimia 50

0
36

Gharama ya kununua samaki inatarajiwa kupanda kwa asilimia 50 nchini Kenya iwapo Bunge litaidhinisha pendekezo la kuanzisha ushuru wa KSh 100,000 [TZS milioni 1.7] kwa tani ili kukinga soko la ndani dhidi ya uagizaji wa bei nafuu kutoka China.

Chama cha Waagizaji, Wachakataji na Wasafirishaji wa Samaki nchini Kenya wanataka ushuru uliopendekezwa ufutwe ili kuruhusu uagizaji wa samaki bila ushuru kwa matumizi ya binadamu kwa miaka mitatu ili kukidhi mahitaji ya sasa na kuongeza kiwango cha matumizi ya samaki kwa kila mtu.

“Pendekezo hili litaongeza zaidi bei ya samaki kwa asilimia 50. Kimsingi, bei ya samaki itakuwa imepanda maradufu ikilinganishwa na miezi 20 iliyopita, na kufanya samaki kuwa ghali.

Pendekezo la kutoza ushuru wa samaki kwa KSh100 kwa kilo moja litafanya bei ya samaki kupanda juu na Wakenya kushindwa kuimudu,” John Msafari, Mwenyekiti wa Chama cha Waagizaji Samaki, Wasindikaji na Wasafirishaji wa Samaki nchini Kenya.

Waagizaji hao wamesema takwimu za Idara ya Uvuvi zinaonesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa mahitaji ya tani 350,000 ambazo haziwezi kukidhiwa na nchi kutokana na kwamba ni tani 21,000 pekee zinazoagizwa kutoka nje.

Samaki wanaotoka China wamekuwa wakiuzwa bei nafuu kwa jumla ya Sh250 [TZS 4,268] kwa kilo dhidi ya samaki wanozalishwa nchini humo ambao huuzwa kwa Sh320 [TZS 5,463].

Waagizaji hao wamesema wanatumia KSh5.2 milioni [TZS milioni 88.8] kutua kontena la futi 40 na tani 26 za samaki wa tilapia katika bandari ya Mombasa na kwamba ushuru huo utapandisha bei hadi KSh7.8 milioni [TZS milioni 133.2].

Send this to a friend