Bwawa la Nyerere kuweka historia nyingine wiki ijayo

0
35

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema katika mwaka wa fedha unaokuja wizara itakamilisha ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP) ambapo wiki ijayo litafikisha kiwango cha chini ujazo wa maji kinachoweza kuanza kutumika kwa uzalishaji wa umeme.

Ameyasema hayo leo bungeni mkoani Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara kwa mwaka 2023/24 ambayo ameliomba Bunge lipitishe TZS trilioni 3.048.

“Katika kipindi cha wiki moja kuanzia sasa tutafikia kiwango cha chini cha kuweza kuzalisha umeme, kiwango cha chini ni mita 163 kutoka usawa wa bahari na tumebakiza mita kama mbili kufikia kiwango hicho.” amesema.

Aidha, ameeleza kuwa katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itakamilisha ufungaji wa mitambo ya kuzalisha umeme pamoja na kuhitimisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme na kukamilisha ujenzi wa barabara za kudumu.

Pamoja na hayo, Waziri Makamba amesema uzalishaji wa umeme utakaoanza rasmi katika mwaka ujao wa fedha, utaingizwa katika gridi ya taifa sambamba na umeme wa jua.

“Katika mwaka ujao wa fedha tutafanya tukio jingine kubwa la kihistoria la kuingiza umeme wa Julius Nyerere kwenye gridi ya taifa kwa mara ya kwanza,” ameeleza Makamba.

Send this to a friend