Serikali imesema kazi ya utengenezaji wa vichwa vya treni ya reli ya kisasa (SGR) haukukamilika kwa wakati kutokana na watengenezaji kupata changamoto kupata baadhi ya vipuri ambayo imechangiwa na janga la UVIKO-19 pamoja vita vya Ukraine na Urusi.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kutokana na uchumi kuyumba kutokana na majanga hayo yaliyoikumba dunia, viwanda vingi vinavyozalisha vipuri hivyo havikuwa katika ratiba ya kawaida ya uzalishaji.
Bwawa la Nyerere kuweka historia nyingine wiki ijayo
“Vipuri ambavyo tulitarajia vingefungwa kwenye vichwa vyetu vya treni viwili ni miongoni mwa vipuri ambavyo vimepata madhara kutokana na changamoto hizi, kwa hiyo mtengenezaji wa vile vichwa viwili hakuweza kuleta vichwa mwezi Aprili kama ambavyo tulitarajia, na kwa hivyo imechelewesha kuwasili kwa vichwa hivi hapa nchini Tanzania,” amesema.
Msigwa amesema kutokana na changamoto hiyo Serikali imeshindwa kufanya majaribio kama ambavyo iliahidi ifikapo Mei mwaka huu kwa kuwa vichwa vya mabehewa havijafika nchini.
Aidha, amesema kichwa cha kwanza cha treni ya SGR kitafika nchini Julai mwaka huu, na pindi kitakapofika majaribio yataanza.