Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewatoa hofu wazazi, walezi na vijana kuhusu malezi ya vijana walioitwa kuhudhuria mafunzo ya JKT kwamba ni mahali salama ambapo vijana wanalelewa vizuri kimaadili kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na nchi na si vinginevyo.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajab Mabele katika taarifa yake kwa umma kufuatia kuzuka kwa taharuki zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai mafunzo ya JKT ni mateso, unyanyasaji na udhalilishaji hususani kwa vijana wa jinsia ya kike.
Jenerali Mabele amesema vijana wanapokuwa makambini muda wote wanakuwa chini ya uangalizi makini wa wakufunzi wenye weledi mkubwa na uzoefu wa kuendesha mafunzo hayo, pia kuna baba na mama mlezi (Patron na Matron) katika kila kambi ambaao wana wajibu wa kusimamia ustawi wa vijana hao kwa kipindi chote wanapokuwa makambini.
Aidha, JKT imewaonya watu wote wanaosambaza taarifa za uzushi na uongo kuhusu mafunzo ya JKT kuacha mara moja, na iwapo yeyote atabainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Hata hivyo, JKT imewasisitiza vijana wote walioitwa kuhudhuria mafunzo hayo kwa Mwaka 2023, kuripoti mara moja kwenye kambi walizopangiwa na kwa tarehe zilizopangwa.