Magunia 731 ya bangi yakamatwa Arusha, hekari 308 zateketezwa

0
11

Kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kufanya operesheni nchi nzima ili kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya gunia 731 za bangi kavu pamoja na kuteketeza ekari 308 za mashamba ya bangi.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa Habari, DCEA imesema imefanya operesheni kwa siku mbili mfululizo katika Wilaya ya Arumeru katika vijiji vya Kisimiri juu ambako walikamata gunia 482 na kuteketeza hekari 101 pamoja na Kijiji cha Lesinoni ambapo walikamata magunia 249 za bangi kavu na kuteketeza hekari 207 za mashamba ya bangi, huku tisa wakishikiliwa kujihusisha na matukioa hayo.

Imeeleza kuwa operesheni hiyo iliyofanyika Mei 31 na Juni 01 ni kufuatia taarifa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2022, ambayo ilitaja mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro na Manyara kujihusisha na kilimo cha bangi kwa kiasi kikubwa.

“Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo yote nchini ili kuhakikisha kilimo cha bangi na mirungi kinatokomezwa kabisa, na wananchi kujikita katika kililmo cha mazao mbadala ya biashara na chakula,” imeeleza taarifa.