DP World ni kampuni ya kimataifa ya usafirishaji iliyoko Dubai, Falme za Kiarabu, iliyojikita na usafirishaji wa mizigo, shughuli za bandarini na huduma za baharini pamoja na maeneo ya biashara huria.
Kampuni hii iliundwa mwaka 2005 kwa munganiko wa Mamlaka ya Bandari ya Dubai na Dubai Ports International. DP World inashughulikia makontena milioni 70 ambayo huletwa na taribani meli 70,000 kila mwaka. Hii ni sawa na takribani asilimia 10 ya idadi ya makontena ya kimataifa inayotolewa na vituo vyao 82 vya baharini na nchi kavu vilivyopo katika zaidi ya nchi 40.
Kampuni ya DP World ni kampuni inayokuwa kwa kasi zaidi duniani. Inafanya kazi katika nchi zaidi ya 60 na inaongoza duniani kwa utoaji wa vifaa madhubuti pamoja na suala zima la usimamizi wa bandari.
Mwaka 2016, DP World ilifikia makubaliano ya kusimamia bandari ya Berbera huko Somaliland kwa mkataba wa miaka 30 na kuwa kitovu kikuu cha bidhaa za kutoka Pembe ya Afrika.
Kampuni hii inashirikiana na nchi za Afrika Mashariki katika uendeshaji wa bandari ikiwemo nchi ya Rwanda na DR Congo, ambapo mnamo Desemba 2021 Serikali ya DRC na kampuni ya DP World zilitia saini makubaliano ya kuendeleza bandari ya kwanza ya kina kirefu nchini humo.
“Hii ni siku ya kujivunia na ya kihistoria kwa DRC, kwani maono yetu ya kuendeleza Bandari ya Banana ili kuibadilisha nchi yetu kuwa kitovu cha biashara ya kikanda, inatimia.
Itakuza uchumi wetu kwa kutengeneza nafasi za kazi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kutoa fursa mpya katika ugavi na kuvutia uwekezaji zaidi wa moja kwa moja wa kigeni. Bandari hiyo mpya haitanufaisha Jimbo la Kati la Congo pekee, bali nchi nzima,” alisema Rais wa Jamhuri ya DRC, Félix-Antoine Tshisekedi katika hafla ya utiaji saini na kampuni hiyo.
Kwanini Tanzania imechagua kuingia makubaliano na kampuni ya Dubai kuboresha bandari ya Dar?
Sultan Ahmed bin Sulayem, Mkurugenzi Mtendaji wa DP World, alisema, “Bandari ya Banana itakuwa ya kisasa, ya hadhi ya kimataifa na bila shaka itabadilisha mchezo kwa DRC. Itakapokamilika, itavutia meli kubwa zinazosafiri kutoka Asia na Ulaya, na hivyo kuimarisha ufikiaji wa nchi kwa masoko ya kimataifa na usambazaji wa kimataifa. Tunamshukuru Rais Tshisekedi na Serikali yake kwa kushirikiana na DP World kuendeleza Bandari ya Banana.”
Kwa upande wa Tanzania, Juni 10, mwaka huu Bunge la Tanzania linatarajia kujadili azimo la mkataba wa makubaliano ya uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam baina ya Serikali na Kampuni hiyo ya Dubai (DP World).
Ikiwa bunge litaridhia azimio hilo, itatoa ruhusa kwa Serikali kuanza majadiliano na Kampuni ya DP World, na ikiwa azimio hilo halitoridhiwa basi hakutokuwa na majadiliano baina ya pande hizo mbili.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa ameeleza kuwa waliona umuhimu wa kuongea na DP World kwa sababu mbalimbali, moja wapo ni kwamba sehemu kubwa ya mizigo inayokuja Tanzania inatoka Mashariki ya Kati, Mashariki ya Mbali na ukanda wa Bahari ya Hindi, na mizigo yao mingi kutoka maeneo hayo inakuja kwenye bandari za Afrika Mashariki.