Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeeleza faida ambazo Tanzania itanufaika baada ya bunge kupitisha azimio la mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano kwa ajili ya uendeshaji na uboreshaji wa utendaji wa kazi za bandari ya Dar es Salaam na kuwezesha Serikali kuendelea na hatua zinazofuata za majadiliano.
Akiwasilisha bungeni maelezo ya awali kuhusu mapendekezo hayo, Waziri Makame Mbarawa ametaja faida 14 ambazo Tanzania itanufaika baada ya bunge kuridhia azimio hilo;
1. Kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 kwa sasa mpaka masaa 24. Ushirikiano utapunguza gharama za utumiaji wa Bandari, na matokeo yake itaongeza idadi ya meli zitazokuja Bandari ya Dar es Salaam kutoka meli 1,569 zilizohudumiwa mwaka 2021/22 mpaka kufikia takriban meli 2,950 ifikapo mwaka 2032/33.
2. Kupunguza muda wa ushushaji wa makontena kutoka siku 4.5 mpaka siku 2.
3. Kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka masaa 12 mpaka saa 1 kutokana na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA.
4. Kupunguza gharama ya usafirishaji wa mizigo kutoka nchi za nje kwenda nchi za Jirani.
5. Kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22 hadi kufikia tani milioni 47.57 mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 158.
6. Kuongezeka kwa Mapato ya Serikali yatokanayo na Kodi ya Forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa bandarini kutoka TZS Trilioni 7.76 za mwaka 2021/22 hadi TZS trilioni 26.7 za mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 244.
7. Kuongezeka kwa ajira zinazotokana na shughuli za bandari kutoka 28,990 mwaka 2021/22 hadi ajira 71,907 ifikapo mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 148.
8. Maboresho ya maeneo ya kuhudumia shehena ya makasha na kuweka mitambo yenye teknolojia ya kisasa.
9. Kuendeleza eneo la kuhifadhia mizigo la bandari kavu kwa kuweka miundombinu ya kisasa ya kuhudumia aina zote za shehena.
10. Maboresho ya magati ya kuhudumia majahazi na abiria ikiwa ni pamoja na kushawishi uingiaji wa meli kubwa za kitalii zitakazo ongeza idadi ya watalii nchini na kuongeza pato la Taifa.
11. Kusimika mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya shughuli za bandari na kuwaunganisha wadau wake.
12. Mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa TPA katika Bandari zote (knowledge and skills transfer).
13. Uanzishwaji wa maeneo maalum ya kiuchumi/viwanda.
14. Kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi zikiwemo Sekta ya Kilimo, mifugo na uvuvi, kuchagiza shughuli za viwanda na biashara, kuchagiza ukuaji wa sekta ndogo za usafirishaji kwa njia ya reli (SGR, TAZARA na MGR) na Barabara, Watanzania kunufaika na teknolojia na ujuzi wa uendeshaji wa bandari kisasa na kujenga mahusiano ya kidiplomasia.