Watoto wanne wamepatikana wakiwa hai baada ya kunusurika kwenye ajali ya ndege na kukaa kwa siku 40 wakijihudumia katika msitu wa Amazoni kabla ya kuokolewa na wanajeshi nchini Colombia.
Rais wa Colombia amesema kuokolewa kwa ndugu hao, wenye umri wa miaka 13, tisa, minne na mmoja, ni furaha kwa nchi hiyo baada ya jitihada za uokoaji zilizofanyika.
Mama wa watoto hao na marubani wawili walifariki wakati ndege yao ilipoanguka msituni Mei Mosi mwaka huu.
Watoto hao wamedai walitumia unga wa muhogo pamoja na matunda ya msituni kama chakula chao kikuu katika msitu huo ambao umejaa nyoka, mbu na wanyama wengine.
Waziri wa Ulinzi, Ivan Velásquez amewaambia waandishi wa habari kuwa watoto watabakia hospitali angalau kwa wiki mbili wakipatiwa matibabu.