Chama cha ACT- Wazalendo kimetoa mapendekezo kwa serikali kuhusu suala la mkataba wa ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na Dubai juu ya usimamizi wa shughuli za bandari ambapo kimetaka wawekezaji hao kuanzisha kampuni ya uendeshaji wa bandari nchini ambayo itakuwa na umiliki wa asilimia 50 kwa 50 kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kampuni ya DP World.
Akizungumza Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kampuni hiyo inaweza kuitwa Tanzania-Dubai Ports Limited (TDPL) ambayo uwepo wake utasaidia kuondoa hofu kwa wananchi pamoja na Tanzania kuwa na udhibiti wa kila kitu katika uwekezaji huo.
Pendekezo la pili, imetaka mkataba wa uendeshaji wa bandari uingiwe kati ya TPA na Kampuni hiyo ya Ubia (TDPL) ambayo itatoa asilimia 50 kwa 50 ili kuhakikisha maslahi ya nchi yanalindwa.
Ifahamu DP World kampuni inayotaka kusimamia Bandari ya Dar
“Tunataka asilimia 50 katika kampuni ya uendeshaji, tunataka makubaliano yote ambayo nchi yetu itaingia na wawekezaji yapitie hiyo kampuni ambayo TPA ina asilimia 50 na mwekezaji ana asilimia 50. Mwekezaji analeta hela na teknolojia, sisi tunatoa bandari yetu na ardhi yetu, 50 kwa 50 wawekeze tuongeze ufanisi ambao unatakiwa katika nchi yetu,” amesema.
Chama hicho pia kimependekeza kampuni ya DP World isifanye uwekezaji wowote kwenye bandari shindani na bandari za Tanzania hususani bandari za nchi jirani bila kujadiliana na Serikali ya Tanzania (exclusivity).