Watu 25 wameuawa na wengine nane wamejeruhiwa kufuatia shambulizi la kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF) katika Shule ya Sekondari Lhubiriha huko Magharibi mwa Uganda.
Jeshi la Polisi nchini humo limesema shambulio hilo lililofanyika Ijumaa lilitekelezwa na kundi la Uganda lenye makao yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Hadi sasa miili 25 imepatikana kutoka shuleni na kuhamishiwa katika Hospitali ya Bwera. Bweni la shule hiyo lilichomwa na ghala la chakula liliporwa wakati wa shambulio,” ameeleza Msemaji wa Jeshi la Polisi, Fred Enaga.
Kenya: Rais Ruto afufua mpango wa ushirikiano na sekta binafsi kuendesha bandari tano
Shambulio hilo dhidi ya shule hiyo iliyoko chini ya kilomita mbili kutoka mpaka wa Uganda na DRC, ni shambulio la kwanza la aina hiyo baada ya shambulio lingine kufanyika miaka mingi iliyopita.
Mnamo Juni 1998, wanafunzi 80 waliteketezwa hadi kufa katika mabweni yao katika shambulio la ADF, kwenye Taasisi ya Ufundi ya Kichwamba karibu na mpaka wa DRC ambapo zaidi ya wanafunzi 100 walitekwa nyara.