Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inafanya tathmini ya utendaji wa mashirika yote ya umma na yale ambayo Serikali ina hisa kubwa, lengo likiwa kubaini mashirika yasiyo na faida ambayo yameshindwa kujiendesha na yanaitia Serikali hasara.
Ameyasema hayo leo katika hafla ya Benki ya NMB kukabidhi gawio kwa Serikali na kusherehekea miaka 25 ya safari ya mafanikio kwa benki hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City mkoani Dar es Salaam.
“Msajili wa hazina amefanya tathmini ya awali ameniletea ripoti nimemwambia nenda kafanye tathmini ya pili, kwa hiyo wale mnaoshika mashirika hapa nendeni kajitazameni vizuri, hii haina kurudi nyuma kuna nitakayoyafuta, kuna nitakayoyasaidia, kuna nitakayoipa miongozo jinsi ya kujiendesha ili wote mfanye faida,” amesema.
Rais Samia atoa onyo kwa wezi wa vifaa miradi ya maendeleo
Aidha, Rais Samia ameipongeza benki ya NMB kwa kuisadia Serikali katika utekelezaji wa huduma mbalimbali za jamii ikiwa ni pamoja na kuboresha vituo vya huduma za afya kama vile hospitali na kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na mchango mkubwa wa ujenzi wa reli ya SGR.
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema benki hiyo imetoa kiasi cha TZS bilioni 2.5 kwa ajili ya ujenzi wa shule ikiwa ni juhudi za kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu katika kutekeleza miradi ya maendeleo.