Wanafunzi 150 wa udaktari kutoka Sudan wahamishiwa Muhimbili

0
25

Wanafunzi 150 wa udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Sayansi na Teknolojia (UMST) cha Khartoum nchini Sudan wamehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kukamilisha mwaka wao wa mwisho wa masomo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema hali ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini Sudan imesababisha kufungwa kwa vyuo na baadhi ya shughuli kusimama, hivyo wanafunzi hao kushindwa kuendelea na ratiba yao ya masomo ya kawaida.

“Wanafunzi hawa wapo mwaka wa tano wa shahada ya kwanza ya utabibu, ambapo katika mwaka huo, mafunzo hufanyika kwa vitendo zaidi, hivyo madaktari hawa wanafunzi watafanya mzunguko (Rotation) katika idara mbalimbali ikiwemo idara ya upasuaji chini ya usimamizi wa madaktari bingwa ili kuhakikisha wanapata maarifa yanayotakiwa” amesema Prof. Janabi

Ishara 9 zinazoashiria una tatizo la afya ya akili

Amebainisha kuwa MNH itatoa fursa kwa wataalamu hao kujifunza kama ambavyo inatoa kwa wataalamu wengine wa ndani na nje ya nchi, na hata baada ya kumaliza masomo yao kama watapendelea kufanya mafunzo tarajali (Intenship), MNH itawapa nafasi hiyo.

Naye, Makamu Mkuu wa chuo cha UMST, Prof. Mamoun Homeida amesema amefurahi kuona wanafunzi kutoka chuo anachokisimamia wamepokelewa vizuri na kwamba ushirikiano huo umetokana na mahusiano ya kindugu yaliyopo baina ya Tanzania na Sudan.

Send this to a friend